Usalama Wako

Tunaupa kipaumbele usalama wa data yako.

Kama data yako si salama, basi si ya faragha. Kwa hivyo, tunahakikisha kuwa huduma za Google, kama vile Tafuta, Ramani na YouTube, zinalindwa na moja ya miundombinu ya usalama ambayo ni thabiti kabisa ulimwenguni.

Usimbaji fiche hudumisha faragha ya data yako inapotumwa

Usimbaji fiche huboresha kiwango cha usalama na faragha kwenye huduma zetu. Unapofanya shughuli kama vile kutuma barua pepe, kushiriki video, kutembelea tovuti au kuhifadhi picha zako, data unayozalisha hutumika kwenye kifaa chako, huduma za Google na vituo vyetu vya data. Tunalinda data hii kwa kutumia vidhibiti vingi vya usalama, ikiwa ni pamoja na teknolojia maarufu ya usimbaji fiche kama vile HTTPS na TLS.

Miundombinu yetu ya wingu hulinda data yako wakati wote

Kuanzia kwa vituo maalum vya data hadi kebo za nyuzi baharini ambazo husafirisha data kati ya mabara, Google hutumia moja ya miundo ya wingu ambayo ni thabiti na salama zaidi ulimwenguni. Miundo hii huchunguzwa kila wakati ili kulinda data yako na kuiwasilisha unapoihitaji. Kwa hakika, tunasambaza data kati ya vituo vingi vya data, ili kukitokea moto au janga fulani, data hiyo itaweza kuhamishwa kiotomatiki na kwa urahisi hadi mahali salama.

Utambuzi wa hatari husaidia kulinda huduma zetu

Tunachunguza huduma na miundombinu yetu kila wakati ili kuilinda dhidi ya hatari, kama vile barua taka, programu hasidi, virusi na aina nyingine za misimbo hasidi.

Hatuzipi serikali idhini ya kufikia data yako moja kwa moja

Hatuwapi kwa siri watu wengine idhini ya kufikia data yako au seva zetu zinazohifadhi data hiyo. Hii inamaanisha kuwa hakuna huluki ya serikali, Marekani au kwingineko, iliyo na idhini ya kufikia maelezo ya wateja wetu moja kwa moja. Wakati mwingine, vituo vya sheria huomba idhini ya kutumia data ya wateja. Timu yetu ya wanasheria hukagua maombi haya na kuyakataa ikiwa hayana msingi wowote au hayakufuata utaratibu unaofaa. Tumejitahidi kufichua maombi haya katika Ripoti yetu ya Uwazi.

Usimbaji fiche umetumiwa kwenye picha ya Eiffel Tower

Usimbaji fiche wa Gmail hutunza faragha ya barua pepe

Kuanzia mwanzo, Gmail imekuwa ikitumia miunganisho iliyosimbwa kwa njia fiche, ambayo huzuia wavamizi wa programu kusoma barua pepe unazotuma. Gmail pia hukutahadharisha dhidi ya hatari za kiusalama, kama vile unapopokea barua pepe ambayo haikutumwa kupitia muunganisho uliosimbwa kwa njia fiche.

Bahasha ya Barua Pepe ya Gmail inaweka ishara ya onyo la kikaguzi cha usalama

Ulinzi dhidi ya barua taka kwenye Gmail huchuja barua pepe zinazoshukiwa kuwa hatari

Mashambulizi mengi ya programu hasidi na kuhadaa ili kupata maelezo ya kibinfasi huanza kwa barua pepe. Usalama wa Gmail hukulinda kutoka kwa taka, kuhadaa ili kupata maelezo ya kibinafsi, na programu hasidi vyema kuliko huduma nyingine yoyote ya barua pepe. Gmail hukagua miundo inayotokana na mamilioni ya barua pepe ili kutambua sifa za barua pepe ambazo watumiaji wameripoti kuwa taka, kisha hutumia sifa hizo kuzuia barua pepe hatari kabla ya kufikia kikasha chako. Unaweza kutusaidia kwa kuchagua "Ripoti Barua Taka" kuhusu barua pepe unazoshuku kuwa hatari.

Mafunzo ya mitambo na akili bandia(AI) husaidia kichujio cha barua taka katika Gmail kuwa sahihi zaidi. Kwa sasa, kinazuia barua taka kufikia kikasha chako kwa asilimia 99.9.

Kivinjari cha Chrome chenye taarifa ya usasishaji wa usalama

Chrome husasisha kiotomatiki usalama wa kivinjari chako

Teknolojia za usalama hubadilika kila wakati. Hivyo basi, unapaswa kupata habari kuhusu usalama kila wakati ili kuzuia madhara. Kwa sababu hiyo, Chrome hukagua kila mara kuhakikisha kuwa toleo la kivinjari unachotumia kimepakiwa zana mpya zaidi za kurekebisha hitilafu za kiusalama, ulinzi dhidi ya programu hasidi na tovuti zinazopotosha na nyinginezo. Chrome hujisasisha kiotomatiki. Kwa hivyo, utalindwa kila wakati na teknolojia ya usalama ya Chrome ya hivi karibuni.

Programu hatari inaingia kwenye kifaa

Google Play huzuia programu hatari kufikia simu yako

Moja ya athari kubwa zaidi za kiusalama kwenye kifaa chako inaweza kuwa programu unazosakinisha. Mfumo wetu wa utambuzi huripoti programu ambazo zinaweza kuwa hatari kabla ya kuwekwa katika Duka la Google Play. Kama hatuna hakika ikiwa programu ni salama, programu hiyo hukaguliwa na wanachama wa Timu ya Ulinzi wa Android. Tunapoboresha mfumo wetu wa utambuzi, tunakagua upya programu ambazo tayari ziko katika Duka la Google Play na kuondoa zile ambazo zinaweza kuwa hatari ili zisifikie kifaa chako.

Google huzuia matangazo yanayopotosha

Shughuli zako mtandaoni zinaweza kuathiriwa na matangazo ambayo yana programu hasidi, yanayofunika maudhui unayojaribu kuangalia, yanayokuza bidhaa bandia au yanayokiuka kwa njia moja au nyingine sera zetu za matangazo. Tunachunguza tatizo hili kwa makini. Kila mwaka, juhudi za wakaguzi wetu na programu thabiti huzuia takribani bilioni moja ya matangazo mbaya. Pia, tunakupa zana za kuripoti matangazo yanayoudhi na kudhibiti aina za matangazo unayoona. Na tunachapisha kila wakati maarifa na mbinu za kuboresha usalama wa intaneti kwa manufaa ya kila mtumiaji.

Vidokezo maarufu vya kukusaidia uimarishe usalama mtandaoni

Imarisha usalama wa akaunti na data yako mtandaoni ukitumia vidokezo hivi vya haraka.

  • Linda vifaa vyako

  • Zuia majaribio ya programu zinazoiba data ya binafsi

  • Vinjari intaneti kwa njia salama

Orodha na Ngao ya Usalama wa Google

Tunga manenosiri thabiti

Kutunga nenosiri salama na thabiti ndiyo hatua muhimu zaidi ambayo unaweza kuchukua ili kulinda akaunti zako mtandaoni. Unaweza kufanya hivyo kwa kutumia maneno mbalimbali ambayo huwezi kuyasahau, lakini ambayo si rahisi kukisiwa na wengine. Unaweza pia kuchukua sentensi ndefu na utunge nenosiri ukitumia herufi za kwanza za kila neno. Ili kuhakikisha kuwa nenosiri ni thabiti zaidi, hakikisha kuwa lina urefu wa angalau herufi nane, kwa sababu nenosiri refu huwa thabiti zaidi.

Ikiwa utaulizwa uweke majibu ya maswali ya usalama, unaweza kutumia majibu bandia ili yasiwe rahisi kukisiwa.

Usiwahi kutumia nenosiri sawa mara mbili

Tumia manenosiri ya kipekee kwa kila akaunti

Hatua ya kutumia nenosiri sawa kuingia katika akaunti nyingi, kama vile akaunti ya Google, wasifu wa mitandao jamii na wavuti za biashara, huongeza uwezekano wa kuathiriwa. Ni sawa na kutumia ufunguo mmoja kufungua nyumba, gari na ofisi – ikiwa mtu atapata ufunguo huo, ataweza kufungua sehemu hizo zote.

Fuatilia manenosiri mengi

Kidhibiti cha nenosiri, kama vile Smart Lock ya Google katika kivinjari cha Chrome, hukusaidia kulinda na kufuatilia manenosiri mbalimbali ya akaunti zako mtandaoni. Kinaweza pia kufuatilia majibu ya maswali ya usalama, na kukutungia manenosiri kwa njia nasibu.

Jilinde dhidi ya wavamizi ukitumia Uthibitishaji wa Hatua Mbili

Uthibitishaji wa Hatua Mbili husaidia kuzuia mtu yeyote ambaye hastahili kufikia akaunti yako kwa kukuhitaji utumie njia ya pili kando na jina la mtumiaji na nenosiri ili kuingia katika akaunti. Kwa mfano, ukiwa na Google, njia hii inaweza kutekelezwa kupitia nambari yenye tarakimu sita iliyoundwa na programu ya Kithibitishaji cha Google au kiashiria katika programu ya Google cha kukuomba uidhinishe ombi la kuingia katika akaunti kutoka kifaa unachokiamini.

Kwa ulinzi zaidi dhidi ya programu zinazoiba data ya binafsi, unaweza kutumia Ufunguo halisi wa usalama ambao huwekwa katika mlango wa USB wa kompyuta yako au kuunganishwa kwenye kifaa chako cha mkononi ukitumia NFC (Mawasiliano ya Vifaa Vinavyokaribiana) au Bluetooth.

Sasisha programu yako

Ili ujilinde dhidi ya hatari za usalama, hakikisha kuwa kila wakati unatumia programu zilizosasishwa kwenye kivinjari, mfumo wa uendeshaji, programu-jalizi au vihariri vyako vya hati. Unapopokea arifa za kusasisha programu yako, hakikisha kuwa umeisasisha haraka iwezekanavyo.

Kagua programu unayotumia mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa unatumia matoleo mapya zaidi. Baadhi ya huduma, kama vile kivinjari cha Chrome, zitajisasisha kiotomatiki.

Tumia kipengele cha kufunga skrini

Wakati hutumii kompyuta, kompyuta ndogo, kompyuta kibao au simu, funga skrini ya kifaa chako ili kuwazuia watu wengine wasitumie kifaa hicho. Ili kuimarisha usalama, weka mipangilio inayoruhusu kifaa chako kujifunga kiotomatiki wakati kiko katika hali tuli.

Funga simu yako ikipotea

Ikiwa simu yako imepotea au kuibwa, tembela Akaunti Yangu na uchague "Tafuta Simu Yako" ili ulinde data yako kwa kufuata hatua chache za haraka. Iwe una kifaa kinachotumia iOS au Android, unaweza kutambua mahali simu yako ilipo na kuifunga kutoka mbali ili mtu yeyote asiifikie na kutumia maelezo yako ya binafsi.

Kivinjari kinaonyesha manenosiri yaliyolindwa katika Chrome

Zuia programu zinazoweza kuwa hatari ili zisifikie simu yako

Hakikisha kuwa umepakua programu ya simu ya mkononi kutoka kwenye chanzo unachokiamini. Ili kuimarisha usalama wa vifaa vya Android, zana ya Google Play Protect hutekeleza ukaguzi wa usalama kwenye programu kutoka Duka la Google Play kabla hujazipakua, na mara kwa mara hukagua kifaa chako ili kubaini ikiwa kuna programu hatari kutoka vyanzo vingine.

Ili kulinda data yako:

  • Kagua programu na ufute zile ambazo hutumii
  • Tembelea mipangilio ya duka la programu na uwashe usasishaji wa kiotomatiki
  • Zipe programu unazoamini pekee idhini ya kufikia data nyeti, kama vile maelezo ya mahali ulipo na picha zako

Kuwa makini kuhusu zawadi, tuzo bandia na ulaghai kupitia barua pepe

Unapaswa kutilia shaka ujumbe kutoka kwa watu usiowajua, haswa unapotiliwa chuku — kama vile kutangaza kuwa umeshinda tuzo fulani, kutuzwa zawadi kwa kukamilisha utafiti au kutangaza njia za haraka za kupata pesa. Usiwahi kubofya viungo ambavyo unatilia shaka na usiwahi kuweka maelezo ya binafsi kwenye utafiti au fomu unazotilia shaka.

Kuwa makini kuhusu maombi ya kufikia maelezo ya binafsi

Usijibu barua pepe, ujumbe wa papo hapo au madirisha ibukizi unayotilia shaka ambayo yanakuomba utoe maelezo ya binafsi, kama vile manenosiri, akaunti ya benki, nambari za kadi za mikopo au hata tarehe yako ya kuzaliwa. Hata kama ujumbe unatoka kwenye tovuti unayoamini, kama vile benki yako, usiwahi kubofya kiungo au kujibu ujumbe huo. Ni heri uende moja kwa moja kwenye programu au tovuti yake ili uingie katika akaunti yako.

Kumbuka kuwa, huduma na tovuti halali hazitatuma ujumbe zikikuomba utume manenosiri au maelezo ya kifedha kupitia barua pepe.

Tahadhari dhidi ya waigaji

Ikiwa mtu unayejua atakutumia barua pepe, lakini ujumbe huo si wa kawaida, huenda akaunti yake imevamiwa.

Angalia mambo yafuatayo:

  • Maombi ya dharura ya pesa
  • Mtu anayedai kuwa amekwama katika nchi nyingine
  • Mtu anayesema kuwa simu yake imeibwa kwa hivyo huwezi kumpigia simu

Usijibu ujumbe au ubofye viungo vyovyote isipokuwa uwe unaweza kuthibitisha kuwa barua pepe ni halali.

Thibitisha faili kabla ya kuzipakua

Baadhi ya wizi wa data unaweza kutokea kupitia viambatisho vya PDF na hati zilizoathiriwa. Ukiona kiambatisho ambacho unatilia shaka, tumia Chrome au hifadhi ya Google ili kukifungua salama na upunguze hatari ya kuathiri kifaa chako. Tukitambua kirusi, tutakutumia ujumbe wa ilani.

Tumia mitandao salama

Tahadhari unapotumia Wi-Fi zisizolipishwa au za umma, hata zile ambazo unahitaji kuweka nenosiri. Ukiunganisha kwenye mtandao wa umma, mtu yeyote aliye karibu anaweza kufuatilia shughuli zako za intaneti kama vile tovuti unazotembelea na maelezo unayoweka kwenye wavuti. Ikiwa huna mtandao mwingine isipokuwa Wi-Fi ya umma au isiyolipishwa, kivinjari cha Chrome kitakujulisha katika sehemu ya anwani ikiwa tovuti hiyo ni salama.

Hakikisha miunganisho ni salama kabla ya kuweka maelezo nyeti

Wakati unavinjari wavuti – haswa unapotaka kuweka maelezo nyeti kama vile manenosiri au maelezo ya kadi za mikopo – hakikisha kuwa muunganisho wa tovuti unazotembelea ni salama. URL salama itaanza kwa HTTPS. Kivinjari cha Chrome kitaonyesha aikoni ya kijani iliyofungwa kwenye sehemu ya URL na kuashiria, "Salama." Ikiwa si salama, itaonyesha "Si Salama." HTTPS husaidia kuimarisha usalama wa shughuli zako za kuvinjari kwa kuunganisha kivinjari au programu yako kwa njia salama kwenye tovuti unazotembelea.