Data Yako

Tunataka uelewe aina ya data tunayokusanya na kutumia.

Unapotumia huduma za Google, unaamini kuwa tutatunza data yako vizuri. Ni wajibu wetu kukufahamisha kuhusu data tunayokusanya na jinsi tunavyoitumia kuboresha huduma zetu kwa manufaa yako.

Zifuatazo ni aina tatu kuu za data ambayo tunakusanya:

Mambo unayofanya

Unapotumia huduma zetu, kwa mfano, kufanya utafutaji kwenye Google, kupata maelekezo kwenye Ramani za Google au kutazama video kwenye YouTube, tunakusanya data hiyo ili kuboresha huduma kwa manufaa yako. Hii inaweza kujumuisha:

 • Vitu unavyotafuta
 • Tovuti unazotembelea
 • Video unazotazama
 • Matangazo unayobofya au unayogonga
 • Mahali uliko
 • Maelezo ya kifaa
 • Anwani ya IP na data ya kidakuzi

Data unayozalisha

Kama umeingia katika akaunti kwa kutumia Google, tunahifadhi na kulinda data unayozalisha kwa kutumia huduma zetu. Hii inaweza kujumuisha:

 • Barua pepe unazotuma na kupokea kwenye Gmail
 • Anwani unazoongeza
 • Matukio ya kalenda
 • Picha na video unazopakia
 • Hati, Majedwali, na Slaidi kwenye Hifadhi

Vitu vinavyokutambulisha wewe kama "wewe"

Unapofungua Akaunti ya Google, huwa tunahifadhi maelezo ya msingi unayotupa. Haya yanaweza kujumuisha:

 • Jina
 • Anwani ya barua pepe na nenosiri
 • Siku ya kuzaliwa
 • Jinsia
 • Nambari ya simu
 • Nchi
Ramani za Google kwenye simu mahiri

Jinsi Ramani za Google zinavyokuelekeza kwa haraka

Unapotumia programu ya Ramani za Google, simu yako hutuma data isiyokutambulisha, ambayo inahusu mahali ulipo, kwenye Google. Data hii hujumuishwa na data kutoka kwa watu waliokaribu nawe ili kutambua hali za trafiki. Kwa mfano, Ramani huweza kutambua wakati magari yanapokwenda polepole kwenye barabara ulipo na kukufahamisha kuwa kuna msongamano mkubwa wa magari. Kwa hivyo, wakati huduma ya Ramani itakapokuarifu kuhusu ajali na kukuelekeza kwenye barabara nyingine ya haraka, huwa tunatumia data ya madereva wengine kukuonyesha njia ya mkato.

Upau wa Tafuta na Google ulio na kipengele cha kukamilisha kiotomatiki

Jinsi Google inavyokamilisha kiotomatiki utafutaji unaofanya

Je, unajua kuwa unapoendeleza neno vibaya, Google itakisia unachokusudia? Zana yetu ya kusahihisha tahajia hutumia data kutoka kwa watu ambao walifanya kosa kama hilo, ili kukurekebishia neno hilo. Hivyo ndivyo tunavyotambua unapoandika "Mobasa," badala ya "Mombasa."

Historia ya mambo uliyotafuta pia inaweza kusaidia Google ikamilishe kiotomatiki hoja unayotafuta. Kama umewahi kutafuta "ndege za kwenda Barcelona", tunaweza kupendekeza kauli hii katika kisanduku cha kutafutia kabla hujamaliza kuiandika. Au kama wewe ni shabiki wa klabu ya soka na mara nyingi hutafuta "alama za Barcelona," huenda tukakuonyesha hizo mara moja.

Kichupo cha Chrome chenye fomu iliyojazwa kiotomatiki

Jinsi Chrome inavyojaza fomu kwa niaba yako

Kila wakati unapofanya ununuzi au kujisajili katika akaunti mtandaoni, wewe hutumia muda mwingi kuweka maelezo ya kibinafsi kwenye fomu. Unapotumia Chrome, tunaweza kuhifadhi maelezo kama vile jina, anwani, nambari ya simu, anwani ya barua pepe na maelezo yako ya malipo, ili tukukamilishie kiotomatiki fomu hizi. Unaweza kubadilisha sehemu mahususi zilizokamilishwa kiotomatiki au uzime mipangilio ya kukamilisha kiotomatiki.

Upau wa Tafuta na Google ulio na kitufe cha matokeo ya faragha na picha ya wasifu

Jinsi huduma ya Tafuta na Google inavyokusaidia kupata maelezo yako

Programu ya Tafuta na Google inaweza kuleta maelezo muhimu yaliyo kwenye Gmail, Picha za Google, Kalenda na zaidi, na kuyaonyesha kwenye matokeo ya utafutaji wa faragha kwa hivyo inakupunguzia kazi hiyo. Tafuta tu mambo kama vile "miadi yangu ya matibabu," "nionyeshe picha nilizopiga ufukoni," au "hoteli nilipohifadhi nafasi." Ikiwa umeingia katika akaunti, utapata maelezo haya kutoka huduma zingine za Google na kuyapata kwa haraka.

Viputo vya gumzo kati ya mtumiaji na Mratibu wa Google

Jinsi Mratibu wa Google anavyoweza kukusaidia kufanya mambo

Mratibu wa Google yuko tayari kukusaidia popote ulipo: nyumbani au safarini. Unapomuuliza Mratibu swali au kumwambia afanye kitu, atatumia data kutoka huduma zingine za Google ili kukupa unachotaka. Kwa mfano, ukiuliza, "Ni mikahawa gani iko karibu?" au "Hali ya anga itakuwaje kesho?", Mratibu wako atatumia data kutoka kwenye Ramani za Google na Tafuta na Google, na data ya mahali ulipo, mambo yanayokuvutia na mapendeleo yako, ili kukupa jibu linalofaa. Unaweza kutembelea zana ya Shughuli Zangu ili uangalie au ufute data ambayo imekusanywa kutokana na jinsi unavyotumia Mratibu.

Kivinjari kinachoonyesha Akaunti Yangu

Dhibiti mipangilio yako ya faragha katika Akaunti Yangu

Ikiwa una Akaunti ya Google au huna, unaweza kubainisha aina ya data inayoweza kuboresha huduma za Google kwa manufaa yako. Kipengele cha Akaunti Yangu hukuruhusu kufikia haraka zana zinazokusaidia kudhibiti maelezo yako ya kibinafsi na kulinda faragha yako.

Utafutaji wa awali katika kidirisha cha Chrome

Angalia aina ya data iliyo katika akaunti yako kwenye Shughuli Zangu

Sehemu ya Shughuli Zangu ni mahali ambapo unaweza kupata kila kitu ambacho umetatufa, kuangalia na kutazama kwa kutumia huduma zetu. Ili uweze kukumbuka mambo uliyotafuta awali mtandaoni kwa urahisi, tunakupa zana za kutafuta kulingana na mada, tarehe na bidhaa. Unaweza kufuta kabisa shughuli mahususi au hata mada zote ambazo huhitaji katika akaunti yako.

Aikoni ya Chrome katika Hali Fiche

Vinjari mtandaoni katika hali ya faragha ukitumia hali fiche

Historia yako ya wavuti inaweza kuboresha matokeo ya utafutaji lakini wakati mwingine ungependa kuvinjari kwa faragha. Kwa mfano, kama unashiriki kompyuta na rafiki yako, pengine hutaki historia yako ya kuvinjari ifichue zawadi unayotafuta. Kama ungependa kufanya utafutaji kama huu, fungua kidirisha fiche kwenye kompyuta au kifaa chako cha mkononi ili kuzuia Google Chrome kuhifadhi historia ya kuvinjari.